Navigate / search

Green Guard,Blue Guard,Red Brigade vinataka kufanana na Imbonerakure

Green Guard

Picha ya Green Guard kwenye Gwaride

Jaji Francis Mutungi,msajili wa vyama vya siasaTanzania Pamoja na mkuu wa jeshi la Polisi,Ernest Mangu wamekutana na upinzani kutoka kwa vyama vya siasa kuhusiana na kupiga marufuku vikundi vya ulinzi vinavyoendelea kuimarika katika vyama hivyo na kuhatarisha amani hasa kuelekea katika uchaguzi mkuu.Akijibu Tuhuma hizo Naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai alisema kuwa vijana wa Green Guard wanapewa mafunzo ya ukakamavu na uzalendo na hawapewi kabisa mafunzo ya kijeshi.

DSC_0037

Picha ya wahitimu wa Red Brigade wakila Kiapo

Kwa upande wake mwenyekiti wa CHADEMA Taifa akihutubia mkutano wa hadhara Nzega alisema kuwa hawako tayari kuacha kuwafundisha Blue Guard wao kwani katika nyakati za nyuma vijana wa CCM wa Green Guard waliwavamia na kuwadhuru na Polisi walishindwa kuwasaidia,hivyo wameamua kutengeneza ulinzi wao wenyewe.

Kwa sasa ninafahamu kuna vyama vinne ambavyo katiba zao zinaruhusu vikundi hivi kuwepo;CCM(Green Guard),CHADEMA(Red Brigade),CUF(Blue Guard),ACT-Wazalendo(ACT-Amani).Ni ukweli usiopingika kuwa kila dalili iko wazi kuwa vikundi hivi vinatengeneza majeshi madogo ya vyama na hasa katika kuelekea kipindi hiki cha uchaguzi.

Wakati wa mapambano ya Uhuru katika nchi nyingi za Afrika walianzisha vikundi mbalimbali vya kuwalinda viongozi wake na kuvitumia kushambulia maadui wao.Moja ya vikundi hivyo ni Umkhonto we Sizwe(Mkuki wa Taifa) cha ANC Kilichoanzishwa na Mandela na hapa kwetu TANU walianzisha kikundi cha TANU bantu Group(baadaye kilibadiilka na kuitwa TANU youth League).Vikundi hivi katika mfumo wa chama kimoja vilikuwa na maana na umuhimu lakini baada ya kuingia kwa vyama vingi ukweli ni kuwa malengo yake yalishafifia na badala yake vilitakiwa vikundi vya vijana wanaojifunza ukakamavu wa akili,kujikwamua kiuchumi na sera za vyama na sio kutumia silaha.

Malalamiko ya CHADEMA dhidi ya Green Guard yamejirudia mara kadhaa na hayakupewa uzito kwa haraka kama ilivyotakiwa.Hivi majuzi wakati CHADEMA wanafanya sherehe ya kuhitimu kwa waliopewa mafunzo katika vikundi vyao vya Red Brigade na pia tukio la kukamatwa kwa wafuasi wawili wa chama hicho wakiwa na silaha mbalimbali na barua inayowapa maelekezo ya kwenda kufanya mafunzo limeshtua wengi Zaidi.
Wengi wa vijana wanaohusika katika mafunzo haya ya vijana wa vyama mbalimbali ni wale wasio na kazi na hawana elimu ya kujitosheleza,kwao hii ni kama njia ya ajira.Ila linalotia shaka Zaidi ni namna ambavyo vikundi hivi vinaweza kujiona na mamlaka isiyo na mipaka hasa pale viongozi wao wanaposema wamepewa kazi hiyo na kuchukua nafasi ya jeshi la polisi.

Nchini Burundi kuna kikundi cha vijana cha chama Tawala CNDD-FDD kinachoitwa Imbonerakure(wale waonao mbali) na katika kuelekea uchaguzi kikundi hiki kimeshaanza kuwa tishio kwa Amani ya Burundi.Kikundi hiki kinachokadiriwa kuwa na wanachama 50,000 kimejaa vijana waliohaidiwa kazi endapo chama chao kitashinda uchaguzi na taarifa zilionyesha kuwa jeshi la serikali linawapa mafunzo ya siri na baadhi yao wanamiliki silahaYako maeneo ambayo kikundi hiki kimeweka vizuizi na hata kuthubutu kuwalipisha watu faini kwa makosa mbalimbali wanayofanya.Kiufupi yako maeneo ambapo kikundi hiki nchini Burundi kinaogopwa kuliko hata jeshi la nchi.

Maoni yangu ni kuwa bila kujali kuwa tumechelewa ni muhimu vikundi hivi vikapigwa marufuku mara moja kwani,tunapoelekea uchaguzi mkuu inahatarisha amani yetu na ni rahisi vikundi hivi hata kutumiwa na wenye nia mbaya na nchi yetu kuingia nchini na kufanya maovu.Ni vyema kukumbuka kuwa AL-Shabab kilianza kama kikundi cha vijana cha chama cha mahakama ya kiislamu nchini Somalia.

Viongozi wa siasa ni bora wakumbuke pia,amani ikipotea,wote tutaathirika.Vijana ni lazima watambue kuwa wako wanasiasa wengi ambao hutumia vijana ili kupata nafasi za kisiasa wanazozitaka.Wakati machafuko yatakapotokea,waathirika wengi watakuwa ni vijana hawa wasio na matumaini na viongozi waliowatuma wengi watakuwa nje ya nchi ama sehemu ambazo ni salama zaidi.Vyama vyetu vibakie na asasi rasmi za Vijana(UVCCM,BAVICHA etc) zitakazokuwa chachu za kuandaa viongozi na kusimamia masuala ya vijana katika Taifa na tuachane kabisa na mwelekeo huu wa sasa,ni hatari kwa amani yetu.Natamani wenye dhamana za vyama na serikali wachukue hatamu katika kulitatua hili mapema kwa kuvifuta kabla mambo hayajaharibika.

TUAMUE SASA,TUVIZUIE SASA.

NAIPENDA TANZANIA.

Joel Arthur Nanauka

Leave a comment

name*

email* (not published)

website