Navigate / search

Hatua 3 Za Kukutoa Kwenye Changamoto Unayoipitia Kwa Sasa

Umeshawahi kupitia hali ambayo kila dalili inaonyesha kwamba hautaweza kuinuka tena?Namaanisha mazingira ambayo hata kwa kila anayekuangalia anajua kabisa kuwa hata kama anakutia moyo,hakuna namna unaweza kufanikiwa.Hali hii huwa inaweza kutokea baada ya mtu kuwekeza katika kitu fulani alichokiamini kwa nguvu zote na kisha anakuja kupata hasara ambayo hakuitegemea kabisa,inaweza kutokea pale ambapo mtu uliyempenda sana na kumwamini siku zote anafanya kitu ambacho haukutarajia na kinakuumiza sana moyo,huwa inatokea pale mtu anapopoteza mtu wake wa karibu sana kwa kifo,huwa inatokea pale ambapo unakuwa umefanya kwa bidii kila unachoweza lakini hauoni matokeo,huwa inatokea pale ambapo unaona watu wanaokuzunguka wanafanya kama yaleyale ambayo wewe unayafanya ila hamna matokeo kabisa,huwa inatokea pale ambapo umebakia peke yako na machozi yako hakuna wa kuyafuta,inaweza kutokea pale ambapo umepewa taarifa kuwa ugonjwa wako hauna tiba.

Nimeshawahi kupitia hali kama hii na nakumbuka mawazo ambayo yalikuwa yanapita kichwani kwangu kwa wakati huo.Ninaamini kabisa kama na wewe unapitia katika hali kama hii inawezekana kabisa mawazo kama hayo yanapita pia kwenye kichwa chako hivi leo.Moja ya kitu ambacho kilikuwa kinajirudia kila wakati ni sauti iliyokuwa inasema-“Hapa ndio mwisho wako,hautainuka tena”.Sauti hii iliendelea kwa muda mrefu na kila nilipokuwa najaribu kuishinda ilikuwa inajirudia tena na tena.Nilichogundua kuwa kadiri nilivyokuwa naisikiliza ndivyo kadiri nilivyokuwa nasikia kuishiwa nguvu.

Kitu kikubwa kinachotokea unapoisikiliza sauti hii ni kuwa unaanza kujenga picha za mambo mabaya zaidi (Worst case scenario imagination).Hii ni pale ambapo kama unaumwa basi unaanza kuwaza jinsi utakavyougua hadi kufa,kama hauna pesa ya kulipa pesa unaanza kuona jisni utakavyofukuzwa kwenye nyumba na kutupiwa vitu nje,au wakati mwingine unaanza kuona utakavyofukuzwa kazi ama kufeli mitihani yako.

Hatua ya kwanza unayotakiwa kuichukua ambayo hata mimi ilinisaidia ni kutoruhusu kutumia muda wako kujena hizi picha.Kumbuka kuwa hata watu ambao wanaamua kuchukua maamuzi ya kujiua huwa ni lazima kwanza anajenga picha.Unapojenga picha katika ubungo wako inatengeneza nguvu kubwa ya kukusukuma kuifanya ile picha iwe uhalisia.Jitahidi kila wakati uanpoanza kupata picha za namna hiyo kuzikataa katika akili yako kwa kuanza kufanya kitu kingine ama kujisemesha kwa sauti,usikubali ubongo wako ujenge picha ambayo hautaki itokee.

Hatua ya pili ya muhimu sana ni kuhakikisha kuwa unatafuta mtu ambaye unamuamini ili umshirikishe hofu yako.Kumbuka siku zote kuwa hakuna sababu ya kukaa na kitu ambacho kinakusababishia maumivu kwenye maisha yako wewe mwenyewe.Usikubali kuamini kwamba kila mtu yuko kinyume nawe,tafuta mtu ambaye unamuamini sana kisha amua kumshirikisha yale yanayokusibu.Wakati mwingine inawezekana asiweze kabisa kutatua tatizo ulilonalo lakini kile kitendo cha kujiruhusu kusema,inakuwa tayari ni ukombozi tosha kwenye maisha yako.Usikubali kufa na changamoto yako ukiwa peke yako,angalia na utafute mtu yeyote uanyemuamini na umshirikishe.

Hatua ya tatu katika kujitoa kwenye changamoto kama hizi ni kuhakikisha kuwa haujitengi kabisa na jamii.Mara nyingi tunapopitia matatizo makubwa ya maisha yetu huwa tunaona njia salama  ni kujitenga na watu wote na kutumia muda wote peke yetu.Ingawa hii inaweza kuwa njia nzuri kwa muda mfupi lakini kwa muda mrefu huwa inasababisha msongo wa mawazo na kukusababishia kukata tama zaidi.Mara baada ya kuwa umepata changamoto kubwa kwenye maisha yako,jitahidi kadiri unavyoweza kurudi katika mfumo wako wa kawaida ambao ulikuwa unauishi.

Kadiri unavyochukua muda mrefu kurudi katika shughuli zako za kawaida ndivyo ambavyo unatengeneza mazingira magumu ya kufanikiwa kwako tena.Najua hiki sio kitu rahisi kukifanya lakini ni cha muhimu.Kumbuka kuna mambo ambayo huwezi kuyabadilisha yakishatokea,hivyo huwa haisaidii kukaa katika masikitiko na huzuni kwa miaka nenda rudi kwa kitu ambacho kimeshapita na hauwezi tena kukirekebisha.Siku zote amini katika kuwa na mwanzo mpya hata katika mazingira magumu na matukio mabaya yaliyojitokeza.

Somo kubwa kwenye maisha yangu nililowahi kupata ni kuwa wakati mwingine unapoona umepoteza fursa kubwa kwenye maisha yako,ni kwa faida yako mwenyewe kwani kuna kitu kizuri sana kinakuwa kiko mbele yako.Bila kujali leo uko katika wakati mgumu kiasi gani,nakushauri tumia hatua hizi ili ujitengenezee mwanzo mpya kwenye maisha yako.

See You At The Top

@JoelNanauka

Leave a comment

name*

email* (not published)

website